News Details

Images
Images
  • News

BARAZA LA WAFANYAKAZI LA TCAA 2023 LAFANYIKA MOROGORO

Watumishi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), wamepongezwa kwa kuendelea kufanya Baraza la Wafanyakazi lenye tija lililofanya uamuzi mkubwa wa ununuzi wa Rada nne za kuongozea ndege nchini kwa mapato yake ya ndani.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi Mrope wakati wa  ufunguzi wa Baraza la wafanyakazi la TCAA uliofanyika Aprili 28,2023 mjini Morogoro.

Bw. Mrope aliyezindua Baraza hilo la wafanyakazi kwa niaba ya Mhe George Simbachawene (MB), Waziri Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,ameongeza kuwa licha ya serikali kuchangia sehemu ya ununuzi wake,  bado Rada hizo ni matokeo ya vikao vya Baraza la Wafanyakazi.

Pia ameongeza kuwa,  kufanyika kwa vikao hivyo vya Baraza ni kuimarisha demokrasia mahala pa kazi,na kuwataka wajumbe wa Baraza hilo kurudisha mrejesho kwa watumishi wenzao.

Bw. Mrope katika uzinduzi huo wa Baraza alizindua pia kitabu cha Mapinduzi Makubwa ya TCAA ndani ya miaka sita (2016-2022), na kuhimiza watumishi wa TCAA kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuendelea kutenda kazi kwa ufanisi. 

"Tunatambua umuhimu wa TCAA katika maendeleo ya nchi yetu lakini TCAA inajengwa kuianzia na wewe mtumishi mmoja, nawasihi sana mfanye kazi kwa kushirikiana kila mmoja kwa nafasi yake na inapobidi msaidie mwingine ili kuhakikisha malengo ya taasisi na serikali kwa ujumla yanafikiwa na huduma inatolewa" amesema Bw.Mrope.

Bw. Mrope pia amempongeza Mkurugenzi Mkuu TCAA Bw.Hamza S. Johari kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usanifu na utengenezaji wa njia za angani na taratibu zake(AFPP).

Awali akizungumza Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Hamza S. Johari amesema Mamlaka inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ukiwemo wa Ununuzi wa Rada nne za kuongozea ndege, kuboresha Mfumo wa Masafa ya Mawasiliano wa Sauti baina ya rubani na waongozaji ndege katika vituo vyote vya kuongozea ndege nchini.

Mkurugenzi Johari ameongeza kuwa,vingine ni kuendelea kutolewa kwa mafunzo kwa wataalam wa Usafiri wa Anga.

Na pia Bw. Johari amezitaja baadhi ya changamoto hasa suala la upatikanaji na ucheleweshaji wa upatikanaji wa vibali vya ajira na upandaji wa madaraja kwa Watumishi wa TCAA. Kitendo ambacho kinashusha ari ya Watumishi:

Baraza hilo linafanyika kwa siku mbili ambapo mbali na kujadili masuala kadhaa yanayoihusu TCAA wajumbe wamepata nafasi ya kupiga kura na kumchagua mfanyakazi bora wa Mamlaka kwa mwaka huu wa fedha,ambapo Bw. Goodluck Msangi Meneja Tehama ameibuka kidedea.