Maswali Yaulizwayo Mara kwa Mara
Tafuta Maswali
Leseni – Marubani na Wataalamu wa Usafiri wa Anga

Ili kupata Leseni ya Rubani wa Ndege za Biashara (CPL), unatakiwa: kuwa na umri wa angalau miaka 18; kuwa na Leseni halali ya Rubani Binafsi (PPL); kutimiza masharti ya Cheti cha Utimamu wa Mwili  Daraja la 1; kukusanya angalau saa 200 (muda) za urushaji ndege; kufaulu mitihani ya nadharia inayotakiwa kikanuni; na kufaulu mtihani wa vitendo wa urubani.

Leseni za marubani zinahitaji kuhuishwa kwa vipindi maalumu. Leseni za CPL na ATPL zinahuishwa kila mwaka kwa wenye leseni walio chini ya umri wa miaka 40, au kila baada ya miezi sita kwa marubani walio na zaidi ya miaka 40. Vilevile, Viwango vya Uwezo wa Urushaji na Utuaji wa Ndege kwa Kutumia vifaa huhitaji kuhuishwa kila baada ya miezi 12. Maelezo kamili kuhusu taratibu za kuhuisha leseni zinapatikana katika kanuni za Mamlaka zinazopatikana katika tovuti.

Ili kubadilisha leseni ya urubani ya kigeni kuwa leseni ya Tanzania, unatakiwa kuwasilisha leseni yako halisi, kitambulisho rasmi, cheti cha utimamu wa mwili, daftari binafsi la kumbukumbu za urushaji ndege, mkataba wa ajira kutoka kwa mwendeshaji wa ndani, pamoja na nyaraka nyingine zinazohitajika. Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania itafanya tathmini na inaweza kuhitaji mitihani au majaribio ya ziada kulingana na aina ya leseni ya nchi ilikotolewa. Inashauriwa kuwasiliana moja kwa moja na Mamlaka kwa mahitaji. Baada ya nyaraka zote kuthibitishwa, mwombaji atatakiwa kutuma maombi mtandaoni kwa ajili ya ubadilishaji wa leseni hiyo.

Ili kuwa mwongoza ndege (Air Traffic Controller – ATC), unatakiwa: kukamilisha mafunzo maalumu katika taasisi ya mafunzo iliyoidhinishwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania; kutimiza masharti ya Cheti cha Utimamu wa Mwili Daraja la 3; kukamilisha mafunzo ya vitendo kwenye kituocha kuongozea ndege; na kufaulu mitihani ya nadharia na vitendo.

Ili kuwa Mhandisi wa Matengenezo ya Ndege (Aircraft Maintenance Engineer – AME), unatakiwa kukamilisha mafunzo ya kiufundi katika taasisi ya mafunzo iliyoidhinishwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, ambayo kwa kawaida huchukua miaka miwili hadi mitatu. Baada ya hapo unatakiwa kufaulu mitihani ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, kupata uzoefu wa vitendo, na kupewa leseni ya AME kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania. Kuna makundi mbalimbali ya leseni kulingana na aina ya kazi inayofanywa, kama vile kiunzi cha ndege (Airframe), injini, vifaa vya kielektroni vya ndege (avionics), na nyinginezo.

Wahudumu wa ndani ya ndege wanatakiwa kukamilisha mafunzo katika taasisi iliyoidhinishwa na Mamlaka, ikiwamo mafunzo ya taratibu za dharura, huduma na usimamizi wa abiria. Baada ya mafunzo hayo hupewa Cheti cha Mhudumu wa Ndani ya Ndege (Cabin Crew Certificate). Mafunzo hayo yanapaswa kuhuishwa mara kwa mara, na mashirika ya ndege yana jukumu la kuhakikisha wahudumu wao wote wana vyeti halali wakati wote.

Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) linahitaji kiwango cha chini cha Umahiri wa Lugha ya Kiingereza cha Daraja la 4 kwa marubani wote wanaofanya safari za kimataifa pamoja na waongoza ndege. mawasiliano. Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania huhakikisha kwamba marubani wote wanaowasiliana kupitia mawimbi ya redio wanatimiza kiwango hiki.

Mitihani hutegemea aina ya leseni inayombwa. Kwa kawaida hujumuisha mitihani ya nadharia katika masomo yafuatayo: Sheria za Anga; Uongozaji ndege; Hali ya Hewa; Maarifa ya Jumla ya Ndege; Utendaji na Mifumo ya Ndege; Utendaji wa Binadamu; na Mawasiliano. Pia, kuna mtihani wa vitendo wa ujuzi wa urubani (flight test) unaosimamiwa na mkaguzi aliyeidhinishwa na Mamlaka.

TCAA hutoza ada mbalimbali kwa leseni na huduma zake, zikiwemo ada za mitihani, ada za kushughulikia maombi, ada za utoaji wa leseni, pamoja na ada za kuhuisha leseni. Ratiba ya sasa ya ada inapatikana kwenye tovuti ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga au kwa kuwasiliana moja kwa moja na ofisi za TCAA. Ada zinaweza kubadilika, hivyo ni muhimu kuthibitisha viwango vya karibuni kabla ya kufanya malipo.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania hutoa aina mbalimbali za leseni za urubani, zikiwamo: Leseni ya Rubani Mwanafunzi (SPL) kwa wanafunzi wa urubani; Leseni ya Rubani Binafsi (PPL); Leseni ya Rubani wa Ndege za biashara (CPL); (ikiwamo abiria na mizigo) Leseni ya Rubani wa Shirika la Ndege (ATPL); Leseni ya Rubani wa Ndege zisizo na Rubani Ndani (RPL) kwa waendesha RPAS; Leseni maalumu kwa aina mbalimbali za ndege kama helikopta na ndege zisizo na injini (gliders).

Ili kuwa rubani mwenye leseni nchini Tanzania, unatakiwa kukamilisha mafunzo katika taasisi ya mafunzo ya usafiri wa usafiri wa anga iliyoidhinishwa na Mamlaka, kutimiza masharti ya umri na vipimo vya utimamu wa mwili, kukusanya saa (muda) zinazohitajika za urushaji ndege, kufaulu mitihani ya nadharia na vitendo iliyowekwa na Mamlaka, pamoja na kuonyesha uwezo wa lugha ya Kiingereza katika kiwango kinachotakiwa. Baada ya hapo unatuma maombi rasmi ya leseni kwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania.

Ili kupata Leseni ya Rubani Binafsi (PPL), unatakiwa: kuwa na umri wa angalau miaka 17; kutimiza masharti ya Cheti cha Utimamu wa Mwili Daraja la 2; kukusanya angalau saa 45 (muda) za urushaji ndege ikiwamo saa 10 (muda) za kuruka peke yako; kufaulu mitihani ya nadharia inayotakiwa kikanuni; na  kufaulu mtihani wa vitendo unaosimamiwa na mkaguzi aliyeidhinishwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania.

Marubani wanatakiwa kuwa na cheti cha utimamu wa mwili kinachotolewa na Mkaguzi wa Utimamu wa Mwili aliyeidhinishwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (Authorized Medical Examiner – AME). Kuna madaraja matatu ya vyeti hivyo: Daraja la 1 kwa marubani wa ndege za biashara; Daraja la 2 kwa marubani wenye Leseni ya Rubani Binafsi (PPL); Daraja la 3 kwa waongozaji ndege na marubani wa ndege zisizo na rubani.
Droni

Ndiyo. Shughuli zote za uendeshaji wa droni nchini Tanzania zinahitaji idhini na kibali kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, bila kujali kama droni inatumika kwa biashara, utafiti, shughuli za serikali, au matumizi binafsi ya burudani.

Mamlaka yaUsafiri wa Anga Tanzania inadhibiti makundi yote ya droni kulingana na uzito wake, madhumuni ya matumizi na eneo la kuruka. Makundi hayo ni pamoja na:  Hatari Ndogo: shughuli zake hufanyika ndani ya mipaka maalumu iliyowekwa; Hatari ya Kati / Hatari Ndogo Inayodhibitiwa: shughuli zake huhitaji masharti maalumu ya udhibiti; Linalohitaji uthibitisho rasmi wa ubora wa kuruka: kundi hili hushughulikiwa kwa utaratibu sawa na ndege zinazoendeshwa na marubani.

Ndiyo. Droni haziruhusiwi kuendeshwa karibu na maeneo yafuatayo: Kambi na vituo vya kijeshi; Ikulu; Maeneo ya magereza; Viwanja vya ndege na maeneo ya kutua ndege (bila kibali maalumu); Majengo na ofisi za serikali (bila kibali maalumu); Hifadhi za taifa (bila kibali maalumu); Maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu (bila kibali maalumu).

Maombi yote ya vibali vya droni hufanywa kupitia mfumo wa mtandaoni wa TCAA. Ili kupata ruhusa ya kuingia kwenye mfumo huo, mwombaji anatakiwa kutuma maombi kupitia barua pepe: drones@tcaa.go.tz Kwa waombaji wasiokuwa wakazi wa Tanzania, maombi yanapaswa kuwasilishwa angalau wiki 3 hadi 4 kabla ya kuingia nchini Tanzania. Kwa waombaji wakazi wa Tanzania, maombi yanapaswa kuwasilishwa angalau wiki 2 kabla

Mchakato wa kupata kibali cha droni huchukua wiki 3 hadi 4 kwa waombaji wasiokuwa wakazi wa Tanzania, na muda mfupi zaidi kwa waombaji wakazi wa Tanzania.

Ndiyo, droni za matumizi ya burudani zinaruhusiwa nchini Tanzania, lakini lazima zizingatie kanuni za Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania Masharti hayo ni pamoja na: kupata kibali cha uendeshaji kutoka TCAA; kurusha droni mbali na viwanja vya ndege na maeneo nyeti; kuzingatia viwango vya juu vya urefu wa kuruka; kutorusha droni usiku bila kibali maalumu; na kuhakikisha usalama wa watu na mali zao.

Ndiyo. Watu binafsi au kampuni za kigeni zinazotaka kuendesha droni nchini Tanzania lazima zipate vibali vya TCAA kabla ya kuwasili nchini.

Droni zinaruhusiwa kuruka hadi urefu wa mita 120 (futi 400) kutoka usawa wa ardhi. Kuzidi kiwango hicho kunahitaji idhini maalumu kutoka TCAA na mara nyingi hatua za ziada za usalama. Maeneo yaliyo karibu na viwanja vya ndege yana viwango vya chini zaidi vya urefu vinavyoruhusiwa.

Kuendesha droni kinyume cha sheria nchini Tanzania kunaweza kusababisha: faini kubwa za fedha; kutaifishwa kwa droni; mashtaka ya jinai; na katika kesi nzito, kifungo gerezani

Ndiyo, Tanzania inahitaji droni zote kusajiliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, na maombi yote ya usajili wa droni hufanywa kupitia mfumo wa mtandaoni wa TCAA.

Ndiyo. Wakati wa kusajili droni, bima ni ya lazima kwa madhumuni ya kulinda dhidi ya hatari kwa watu wengine (third party risks). Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania inawataka waendeshaji wa droni kuwa na bima ya dhima kwa watu wengine inayogharamia uharibifu ambao droni inaweza kusababisha kwa watu au mali.

Ndiyo, droni zinaweza kurushwa katika Hifadhi za Taifa, lakini zitahitaji vibali vya ziada kama kibali kutoka kwa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa. Waombaji wanaotaka kurusha droni ndani ya Hifadhi za Taifa wanashauriwa kuwasiliana mapema na mamlaka za hifadhi husika kwa maelezo zaidi na mwongozo.

Ndiyo, droni haziruhusiwi kuruka usiku bila kibali maalumu kutoka TCAA. Kibali hicho kinahitaji droni kuwa na taa zinazofaa pamoja na mwendeshaji kufuata taratibu maalumu za usalama. Hata kwa kuwa na kibali, kiwango cha juu zaidi cha tahadhari kinahitajika wakati wa shughuli za usiku.

Kwa kawaida, vibali vya droni hutolewa kwa eneo maalumu. Kufanya shughuli katika maeneo mapya kunahitaji idhini ya ziada au marekebisho ya kibali kilichopo.

Ili kufanya upya kibali cha droni, wasilisha ombi la kufanya upya kwa TCAA kabla ya kibali cha sasa kuisha muda wake. Unatakiwa kuthibitisha kuwa taarifa zako na droni yako hazijabadilika (au kutoa taarifa za mabadiliko yoyote yaliyotokea), kulipa ada ya kufanya upya, na kutimiza masharti yote ya sasa ya TCAA. Inashauriwa kuanza mchakato wa kufanya upya mapema ili kuepuka kukosa uhalali wa kibali.

Ndiyo. Maombi yanaweza kukataliwa kutokana na sababu zifuatazo: Nyaraka kutokamilika; Masuala ya kiusalama; Mipango isiyo salama ya uendeshaji; Migongano na maeneo yenye vizuizi vya anga.

Muda wa uhalali wa kibali cha droni hutegemea ombi la mwombaji. Kuna chaguo za vibali vya siku, mwezi, au mwaka.

Kwa msaada wowote, unaweza kutuma maombi kupitia barua pepe ya TCAA: drones@tcaa.go.tz au kupiga simu moja kwa moja kupitia namba: 0800110193

Ndiyo, lakini kwa idhini maalumu. Shughuli yoyote ya droni inayofanyika ndani ya eneo la kilomita 10 kutoka katikati ya uwanja wa ndege hairuhusiwi kufanyika isipokuwa mhusika awe amepata kibali kutoka kwa Udhibiti wa Usafiri wa Anga (Air Traffic Control – ATC).
Uendeshaji wa Safari za Ndege na Vibali

Ndiyo, ndege za kigeni zinazofanya shughuli za kibiashara nchini Tanzania kwa kawaida zinahitaji vibali vya kutua kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania pamoja na idhini kutoka Tanzania Airports Authority (TAA). Vibali hivi vinapaswa kuombwa mapema, kwa kawaida siku chache kabla ya safari ya ndege. Huduma za ratiba maalumu zinazofanywa chini ya makubaliano yaliyoidhinishwa ya huduma za anga kati ya nchi mbili zinaweza kufuata utaratibu tofauti.

Ili kuomba kibali cha kupita katika anga ya Tanzania, mwendeshaji wa ndege au mwakilishi wake (kwa kawaida wakala wa huduma za ardhini) anatakiwa kuwasilisha ombi kwa TCAA au mamlaka ya Huduma za Uongozaji ndege, akitoa taarifa za ndege, njia ya safari, muda wa safari, pamoja na idadi ya abiria na wafanyakazi wa ndege. Kwa kawaida ombi hili huwasilishwa angalau saa 24 kabla ya safari ya ndege.

Nyaraka zinazohitajika kwa kawaida ni pamoja na: Tamko la Jumla la Safari (General Declaration – GenDec); Orodha ya Abiria; Orodha ya Mizigo; Cheti cha Ubora wa Kuruka; Leseni za wafanyakazi wa ndege; Vyeti vya bima; na kwa baadhi ya safari, matamko ya bidhaa hatarishi. Mahitaji yanaweza kutofautiana kulingana na aina ya safari na nchi ambayo ndege imesajiliwa.

Vibali vya kutua na vibali vya kupita katika anga ya Tanzania kwa kawaida hushughulikiwa ndani ya saa 24 hadi 48 kwa maombi yaliyokamilika vizuri. Hata hivyo, inashauriwa kuomba mapema zaidi, hasa kwa safari za msimu wenye shughuli nyingi au safari zinazohusisha maeneo nyeti. Vibali vya dharura vinaweza kushughulikiwa kwa haraka zaidi lakini haviwezi kuhakikishwa.

Cabotage ni haki ya shirika la ndege la kigeni kusafirisha abiria au mizigo kati ya maeneo mawili ndani ya nchi nyingine. Kwa mfano, shirika la ndege la Kenya kusafirisha abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Kilimanjaro International Airport kungehesabika kama cabotage. Kwa kawaida haki hii haitolewi kwa waendeshaji wa kigeni bila makubaliano maalumu, na Tanzania hutekeleza kizuizi hicho.

Ndiyo, kama ilivyo kwa nchi nyingi, Tanzania hulinda soko lake la ndani kwa ajili ya mashirika yake ya ndege ya kitaifa. Mashirika ya ndege ya kigeni kwa kawaida hayaruhusiwi kusafirisha abiria katika njia za ndani ya Tanzania bila makubaliano maalumu au idhini ya kipekee. Hii inaendana na mikataba ya kimataifa ya usafiri wa anga pamoja na makubaliano ya huduma za anga kati ya nchi mbili.

Mgao wa nafasi za muda viwanjani ni mfumo wa kugawa muda maalumu wa matumizi ya uwanja kwa kila ndege katika viwanja vyenye msongamano mkubwa wa ndege. Mfumo huu husaidia kusimamia msongamano wa trafiki ya anga na kuhakikisha uendeshaji mzuri wa viwanja vya ndege. Nafasi hizo hugawiwa kwa mujibu wa miongozo ya kimataifa ya International Air Transport Association (IATA Worldwide Airport Slot Guidelines) na husimamiwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania pamoja na Tanzania Airports Authority.

Kutua kwa dharura hushughulikiwa kupitia mfumo wa Udhibiti wa Usafiri wa Anga (ATC) pamoja na viwanja vya ndege vya Tanzania, ambavyo vimeandaliwa kushughulikia hali za dharura. Rubani anayehitaji kutua kwa dharura atawasiliana na ATC kwa kutumia mawimbi rasmi ya dharura kama vile “Mayday” au “Pan-Pan.” Viwanja vya ndege vina vikosi vya Uokoaji na Uzimaji Moto kwa Ndege (Aircraft Rescue and Fire Fighting – ARFF) vilivyo tayari muda wote. Baada ya tukio hilo, TCAA itafanya uchunguzi wa tukio husika.

NOTAMs (Notices to Airmen) ni matangazo rasmi yanayotolewa kwa marubani na waendeshaji wa ndege kuhusu mabadiliko muhimu katika mfumo wa uongozaji ndege. Mabadiliko hayo yanaweza kujumuisha: mabadiliko ya njia za safari; vizuizi vya muda; kazi za ujenzi katika viwanja vya ndege; au hatari nyingine zinazoweza kuathiri usalama wa safari za ndege. NOTAM hutangazwa kupitia mfumo wa kimataifa wa NOTAM na hupatikana kupitia tovuti za anga pamoja na mifumo maalumu ya taarifa za anga.

Kanuni za kawaida za uendeshaji wa safari za ndege nchini Tanzania ni pamoja na: kufuata Kanuni za Kuruka kwa Kutumia Ala (IFR) au Kanuni za Kuruka kwa Kuona (VFR) kulingana na mazingira; mawasiliano ya lazima na Udhibiti wa Usafiri wa Anga (ATC); kuzingatia njia na viwango vya urefu vilivyotolewa; matumizi ya vifaa vya utambuzi wa ndege (transponders); na kuzingatia masharti yaliyowekwa katika Viambatisho husika vya International Civil Aviation Organization (ICAO). Kanuni hizi zimewekwa ili kulinda usalama wa watumiaji wote wa anga ya Tanzania.
Usalama, Ulinzi na Uzingatiaji wa Kanuni

Uchunguzi wa ajali za anga ni mchakato rasmi wa kubaini chanzo cha ajali ya ndege au tukio kubwa la anga. Tanzania ina Kitengo maalumu cha Uchunguzi wa Ajali za Ndege (Air Accident Investigation Unit – AAIU) kinachofanya kazi kwa kujitegemea bila kuingiliwa na TCAA. Lengo la uchunguzi si kulaumu mtu, bali kuzuia matukio yajayo kwa kubaini na kushughulikia udhaifu uliopo katika mifumo ya usalama.

Bidhaa hatarishi zinazosafirishwa kwa ndege hudhibitiwa chini ya Kanuni za Bidhaa Hatarishi za International Air Transport Association (IATA Dangerous Goods Regulations – DGR), ambazo Tanzania huzingatia. Kanuni hizi hubainisha ni vifaa gani hatarishi vinaweza kusafirishwa kwa ndege, namna vinavyopaswa kufungashwa, kuwekewa alama, na kutangazwa. Kampuni zinazoshughulikia bidhaa hatarishi lazima zisajiliwe na kuwapatia wafanyakazi wao mafunzo yanayofaa. Adhabu kali hutumika kwa ukiukwaji wa kanuni hizi.

Adhabu za ukiukwaji wa kanuni za usalama wa anga zinaweza kujumuisha: onyo rasmi; faini za fedha; kusimamishwa kwa muda kwa leseni au cheti; kufutwa kabisa kwa leseni au cheti; au mashtaka ya jinai kwa ukiukwaji mkubwa. Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania ina mamlaka ya kuchukua hatua za haraka pale ambapo kuna tishio la moja kwa moja kwa usalama.

Viwanja vya ndege vya Tanzania vina hatua za kiusalama zinazozingatia Kanuni za Usafiri wa Anga (Usalama) za mwaka 2018 zilizofanyiwa marekebisho, pamoja na Mpango wa Taifa wa Usalama wa Usafiri wa Anga. Hatua hizo ni pamoja na: ukaguzi wa abiria na mizigo yao kwa kutumia mashine za X-ray na vifaa vya kugundua vyuma; ukaguzi wa mwili unaofanywa na maafisa wa usalama; ukaguzi wa wafanyakazi wa anga; ukaguzi wa usalama wa ndege kabla ya safari; na udhibiti wa kuingia katika maeneo ya shughuli za ndege. Usalama huu unasimamiwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania pamoja na Kamati ya Taifa ya Usalama wa Usafiri wa Anga.

Mfumo wa Usimamizi wa Usalama (SMS) ni mfumo unaotambuliwa kimataifa kwa ajili ya kusimamia usalama katika sekta ya usafiri wa anga. Mfumo huu unajumuisha sera, taratibu, na mifumo ya kitaasisi ya kutambua hatari, kutathmini vihatarishi, na kudhibiti vihatarishi hivyo kabla havijasababisha ajali. Mashirika yote ya ndege, viwanja vya ndege, na wadau wengine wa anga nchini Tanzania wanatakiwa kuwa na SMS iliyoidhinishwa na TCAA.

TCAA hufuatilia usalama wa mashirika ya ndege kupitia: ukaguzi wa mara kwa mara wa usalama wa shughuli za ndege; mapitio ya taarifa za matukio; ukaguzi wa kumbukumbu za matengenezo; tathmini ya programu za mafunzo; na ufuatiliaji wa jumla wa utendaji wa mashirika ya ndege. TCAA pia hushiriki katika Mpango wa Kimataifa wa Ukaguzi wa Usimamizi wa Usalama wa ICAO (Universal Safety Oversight Audit Programme – USOAP), ambao hukagua mfumo mzima wa usimamizi wa usalama wa anga wa Tanzania.

Tanzania hutekeleza viwango vya kimataifa vya International Civil Aviation Organization (ICAO) kwa kuvijumuisha katika kanuni za kitaifa za usafiri wa anga, kutoa mafunzo kwa watumishi wa TCAA yanayoendana na viwango hivyo, na kushiriki katika programu za kimataifa za ukaguzi kama ICAO USOAP. Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania pia hushirikiana na mamlaka za usafiri wa anga za nchi jirani na za kimataifa kupitia makubaliano ya ushirikiano.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania hutekeleza viwango vya usalama kupitia: ukaguzi wa mara kwa mara na ukaguzi wa kushtukiza kwa mashirika ya ndege, viwanja vya ndege, na wadau wengine; usimamizi wa leseni na vyeti; ukaguzi wa nyaraka; tathmini ya Mifumo ya Usimamizi wa Usalama pamoja na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanaokiuka kanuni. Mamlaka ina wajibu wa kusimamisha au kufuta leseni pale ambapo usalama utahatarishwa.

Matukio ya usafiri wa anga yanapaswa kuripotiwa kwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania haraka iwezekanavyo baada ya kutokea kwa tukio linalohusika. Marubani, wahudumu wa ndege na wataalamu wengine wa anga wana wajibu wa kisheria wa kuripoti aina za matukio. Taarifa zinaweza kuwasilishwa kwa Mamlaka kwa kutumia fomu rasmi zinazopatikana kwenye tovuti ya Mamlaka au kupitia mawasiliano ya moja kwa moja. Kuripoti mapema husaidia uchunguzi na kusaidia kuzuia matukio kama hayo kutokea tena baadaye.

Wakaguzi wa Usalama na Ulinzi wa Anga wana jukumu muhimu katika kuhakikisha usalama wa usafiri wa anga. Wanafanya shughuli za usimamizi zinazojumuisha: ukaguzi na tathmini za mashirika ya ndege, viwanja vya ndege, na wataalamu wa usafiri wa anga; kuthibitisha uzingatiaji wa kanuni; kutoa mwongozo na mafunzo; kuchunguza matukio na ajali za safari za ndege; na kuwasilisha taarifa za matokeo yao kwa menejimenti ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania Wakaguzi hawa hupewa mafunzo maalumu ya kitaalamu na wanatambuliwa kwa mujibu wa sheria za usafiri wa anga za Tanzania.
Maswali ya Jumla na Taasisi

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania ina jukumu la kudhibiti na kusimamia shughuli zote za usafiri wa anga nchini Tanzania. Hii inajumuisha utoaji wa leseni kwa wataalamu wa usafiri wa anga, viwanja vya ndege, taasisi za mafunzo ya usafiri wa anga na huduma za usafiri wa anga, ukaguzi wa usalama na ulinzi wa usafiri wa anga, utoaji wa huduma za uongozaji ndege, pamoja na kuhakikisha Tanzania inazingatia viwango vya kimataifa vya ICAO.

Usafiri wa anga nchini Tanzania unasimamiwa hasa na Sheria ya Usafiri wa Anga   (Sura ya 80), ambayo inaanzisha Mamlaka ya Usafiri wa AngaTanzania na kuweka mfumo wa kisheria wa tasnia inayohusika. Pia, kuna kanuni mbalimbali zilizotungwa chini ya Sheria hiyo pamoja na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia, ikiwamo Mkataba wa Kimataifa wa Usafiri wa Anga wa Mwaka 1944.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania inasimamia vyote. Inasimamia viwanja vya ndege kwa kuzingatia usalama na viwango vya uendeshaji, ingawa shughuli za kila siku za viwanja vingi vya ndege husimamiwa na waendeshaji wa viwanja hivyo.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ilianzishwa kwa Sheria ya Usafiri wa Anga Cap.80 (R.E 2023) ili kusimamia sekta ya usafiri wa anga nchini.   

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini Tanzania huhakikisha usalama kupitia mbinu mbalimbali, zikiwamo ukaguzi wa mara kwa mara na wa kushtukiza wa huduma zinazosimamiwa; usimamizi wa leseni na vyeti; utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Usalama wa Usafiri wa Anga (SSP); ufuatiliaji wa ajali na matukio ya usafiri wa anga; mafunzo kwa wakaguzi; pamoja na kuhakikisha uzingatiaji wa viwango vya ICAO. Mamlaka pia, hushirikiana na taasisi nyingine za usafiri wa anga kubadilishana taarifa za usalama.

Tanzania ni mwanachama wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) na hutekeleza Viwango na Utaratibu unaopendekezwa (SARPs) uliomo katika Viambatisho vya Mkataba wa Kimataifa wa Usafiri wa Anga wa mwaka 1944. Tanzania pia ni mwanachama wa Kamisheni ya Afrika ya Usafiri wa Anga (African Civil Aviation Commission (AFCAC) na hushirikiana na mashirika mengine ya kimataifa ya anga ili kuhakikisha uzingatiaji wa viwango vya kimataifa.

Makao makuu ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania yapo Dar es Salaam, makutano ya Barabara ya Nyerere na Kitunda, Aviation House. Mamlaka pia ina ofisi 15 katika viwanja vya ndegeTanzania, ambavyo ni Viwanja vya Kimataifa vya Julius Nyerere, Abeid Amani Karume na Kilimanjaro. Viwanja vingine ni; Arusha, Bukoba, Dodoma, Iringa, Kigoma, Mtwara, Mwanza, Pemba, Songea, Songwe, Tabora na Tanga kwa ajili ya kufuatilia kwa karibu shughuli za usafiri wa anga.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania inaendesha njia mbalimbali za mawasiliano ili kuwezesha umma kuwasiliana nayo. Tovuti rasmi ya Mamlaka ni www.tcaa.go.tz, ambapo taarifa kuhusu huduma na masuala ya udhibiti zinapatikana. Mawasiliano kwa njia ya posta yanaweza kutumwa kupitia anwani ya: S.L.P. 2819, Dar es Salaam, Tanzania. Maswali kwa njia ya simu yanaweza kuulizwa kupitia namba: (+255) 22 219 8100, na mawasiliano ya baruapepe yanapatikana kupitia: barua@tcaa.go.tz. Mamlaka pia ina akaunti za mitandao ya kijamii kwenye Instagram, Facebook, X, na LinkedIn kwa jina la @officialtcaa, ambapo taarifa na maboresho kuhusu kanuni na huduma za usafiri wa anga hutolewa.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania hutoa huduma mbalimbali kwa umma, zikiwamo: utoaji wa leseni kwa wataalamu wa usafiri wa anga; usajili wa ndege; kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za usafiri wa anga; utoaji wa vibali vya matumizi ya droni; utoaji wa leseni kwa huduma za usafiri wa anga na ushughulikiaji wa huduma za ardhini; utoaji wa taarifa za usalama na elimu kwa umma; pamoja na NOTAM na taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wa usafiri wa anga.
Leseni za Huduma za Anga na Biashara

Leseni ya Huduma za Usafiri wa Ndege (ASL) ni leseni ya kisheria inayotolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania inayoruhusu kampuni au mtu binafsi kutoa huduma za usafiri wa ndege nchini Tanzania. Leseni ya Huduma za Usafiri wa Ndege inathibitisha kuwa mwombaji ametimiza mahitaji ya kisheria, kifedha na kiusalama ya kuendesha biashara ya usafiri wa ndege. Bila kuwa na Leseni ya Huduma za Usafiri wa Ndege halali, hakuna mtu anayeruhusiwa kutoa huduma za usafiri wa ndege wa kibiashara nchini Tanzania.

Ili kuomba Leseni ya Huduma za Usafiri wa Ndege, mwombaji anatakiwa: kuwasilisha fomu rasmi za maombi za Leseni ya Huduma za Usafiri wa Ndege kwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania; kuthibitisha umiliki wa Kitanzania au umiliki mkubwa wa hisa na wazawa; kuonyesha uwezo wa kutosha wa kifedha; kuwasilisha mpango wa biashara; na kuthibitisha umiliki au nia ya kupata Cheti cha Mwendeshaji wa Ndege (Air Operator Certificate – AOC). Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania itafanya tathmini ya kina kabla ya kutoa Leseni ya Huduma za Usafiri wa Ndege.

Kuanzisha shirika la ndege nchini Tanzania kunahitaji: kuwa kampuni iliyosajiliwa Tanzania; kupata ASL na AOC kutoka Mamlaka; kuonyesha uwezo wa kutosha wa kifedha; kuwa na ndege zenye nyaraka halali; kuajiri wafanyakazi wenye sifa na leseni zinazotakiwa; na  kuzingatia kanuni zote za usalama wa anga.

Kupata leseni ya huduma ya Usafiri wa ndege na cheti cha Uendeshaji wa ndege kunaweza kuchukua kati ya siku tisini hadi mwaka mmoja au zaidi, kutegemea ukamilifu wa maombi na kiwango ambacho mwombaji ametimiza mahitaji yote. Utaratibu huu unahusisha mapitio ya nyaraka, ukaguzi wa moja kwa moja, na tathmini ya shughuli za uendeshaji. Mamlaka itatoa mwongozo wa kina katika hatua zote za utaratibu.

Ada zinazohusika ni pamoja na: ada ya maombi ya leseni ya huduma ya Usafiri wa ndege; ada ya tathmini ya cheti cha Uendeshaji wa ndege; ada za ukaguzi na usimamizi; pamoja na ada za leseni za kila mwaka. Kwa kuwa ada hizi ni kubwa na zinaweza kubadilika, ni muhimu kuwasiliana moja kwa moja na Mamlaka ili kupata viwango vya sasa vya ada na kuelewa wajibu wote wa kifedha unaohusika.

Tanzania inaruhusu ushiriki wa kampuni za kigeni katika tasnia ya usafiri wa anga lakini kwa masharti maalumu. Kwa mujibu wa sheria, mashirika ya ndege ya Tanzania yanatakiwa kuwa na umiliki mkubwa wa Watanzania. Kampuni za kigeni zinaweza kushirikiana na washirika wa Kitanzania au kuwekeza kupitia mifumo inayoruhusiwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania. Mamlaka ya Usafiri wa Anga pamoja na mamlaka nyingine husimamia utekelezaji wa masharti haya ya umiliki.

Leseni ya huduma za shughuli za ardhini inahusu kampuni zinazotoa huduma za kusaidia ndege viwanjani, kama vile: kusaidia upakiaji na upakuaji wa mizigo na shehena; huduma kwa abiria; kuelekeza ndege viwanjani; na huduma za matengenezo ya ndege za muda mfupi. Kampuni hizo lazima zipate idhini ya Mamlaka na kuzingatia viwango vya usalama.

Ndiyo, Ili kuanzisha biashara yoyote katika tasnia ya usafiri wa anga nchini Tanzania, kwanza unatakiwa kubainisha aina ya biashara unayotaka kufanya, kama vile shirika la ndege, shule ya mafunzo ya urubani, matengenezo ya ndege au nyinginezo. Baada ya hapo, unatakiwa kuomba leseni na vibali vinavyohusika kutoka Mamlaka. Pia, utahitaji kusajili kampuni yako kisheria, kutimiza masharti ya majengo na miundombinu yanayotakiwa, pamoja na kuzingatia kanuni zote za usalama zinazohusika.

Huduma za ndege za kukodisha zinahitaji: Leseni halali ya Huduma za Usafiri wa Anga (ASL); Cheti cha Mwendeshaji wa Ndege (AOC) kinachoruhusu shughuli za ndege za kukodisha Kila safari ya kimataifa ya ndege za kukodisha inaweza kuhitaji kibali maalumu kutoka nchi inayokwenda. Mamlaka husimamia uzingatiaji wa masharti yote yanayohusiana na huduma za ndege za kukodisha.

Cheti cha Mwendeshaji wa Ndege ni hati rasmi inayotolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania kuthibitisha kuwa mwendeshaji wa ndege ana uwezo wa kiufundi, kiusalama na kiuendeshaji wa kutoa huduma za usafiri wa anga kwa usalama. Cheti cha Mwendeshaji wa Ndege hubainisha aina za ndege, njia za safari na shughuli zinazoruhusiwa. Cheti hiki lazima kihuishwe na kukaguliwa mara kwa mara.

Kupata Cheti cha Mwendeshaji wa Ndege kunahitaji: kuwasilisha maombi ya kina kwa Mamlaka yakiambatishwa na Mwongozo wa Uendeshaji , Programu ya Matengenezo na nyaraka nyingine muhimu; kufaulu tathmini ya awali; kufaulu ukaguzi rasmi wa Mamlaka; na kufanya safari za majaribio Utaratibu huu ni wa kina na unahitaji ushirikiano wa karibu na Mamlaka katika hatua zote.

Udhibiti wa kiuchumi katika usafiri wa anga unahusisha mambo kama: bei za tiketi na mazingira ya ushindani; vibali vya uendeshaji wa njia za safari za ndege; makubaliano ya huduma za anga kati ya nchi mbili; uwezo wa usafirishaji wa abiria na mizigo; pamoja na ulinzi wa watumiaji wa huduma za anga. Mamlaka husimamia baadhi ya maeneo haya ili kuhakikisha ushindani wa haki na kulinda abiria wa usafiri wa anga.

Tozo za usafiri wa anga nchini Tanzania huamuliwa na mambo mbalimbali kama vile gharama za uendeshaji, bei za mafuta, ushindani wa kibiashara, pamoja na masharti ya makubaliano ya huduma za usafiri wa anga kati ya nchi mbili. Mamlaka ina jukumu la kufuatilia na kuhakikisha kuwa tozo hizo zinaendana na sheria zinazohusika. Hata hivyo, nguvu ya soko pia ina mchango mkubwa katika kupanga bei, hasa kwa safari za kimataifa.
Unahitaji Msaada?