Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mhe. Abdallah Mitawi, ameipongeza Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa juhudi na hatua mbalimbali inazochukua katika kuimarisha usalama na ulinzi wa usafiri wa anga nchini, akisisitiza kuwa usafiri wa anga ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa.
Mhe. Mitawi ametoa pongezi hizo wakati alipotembelea TCAA kwa lengo la kufahamu kwa kina kazi, majukumu na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Mamlaka katika kusimamia, kudhibiti na kuendeleza sekta ya usafiri wa anga nchini.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Dkt. Jabiri Bakari, alimweleza Naibu Katibu Mkuu kuhusu majukumu ya Mamlaka, ikiwemo usimamizi na udhibiti wa shughuli za usafiri wa anga, ulinzi na usalama wa anga, pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali kwa watumiaji wa usafiri wa anga wa sekta hiyo.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mitawi alipata fursa ya kujionea maendeleo ya mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Chuo cha Kisasa cha Usafiri wa Anga (CATC), pamoja na kutembelea Kituo cha TCAA cha Uongozaji ndege kilichopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).