Muhtasari
Iwapo Tanzania ndiyo makao makuu ya biashara yako na unakusudia ndege yako kutoa huduma kwa madhumuni ya usafiri wa anga wa kibiashara kwa umma (kukodi na kulipwa), Kanuni za Usafiri wa Anga Tanzania (Civil Aviation Regulations – CARs) zinakutaka kuwa na Cheti cha Uendeshaji wa Ndege (Air Operator Certificate – AOC) kabla ya kuanza shughuli za uendeshaji.
Ofisi ya Uendeshaji wa Ndege ya Mamlaka ndiyo inayotoa Vyeti vya Uendeshaji wa Ndege (AOCs) kwa watoa huduma za ndege kwa mujibu wa Kanuni za Usafiri wa Anga kuhusu Uthibitishaji na Usimamizi wa Watoa huduma za Ndege za mwaka 2017 [Civil Aviation (Air Operator Certification and Administration) Regulations, 2017].
TANBIHI: Unatakiwa kuwasilisha maombi na kupata kibali cha kiudhibiti (AOC) kutoka TCAA angalau siku tisini (90) kabla ya kuanza kutoa huduma za usafiri wa kibiashara wa anga, iwe ni safari zenye ratiba au zisizo na ratiba.
Majukumu ya Ofisi ya Uendeshaji wa Ndege
Ofisi ya Uendeshaji wa Ndege ya Mamlaka ina majukumu yafuatayo:-
1. UTHIBITISHAJI (CERTIFICATION)
(a) Ofisi ya Uendeshaji wa Ndege kwa kushirikiana na Ofisi ya Ubora wa Ndege Kuruka hufanya uthibitishaji wa awali, ukaguzi wa kushtukiza (Ad-hoc inspections) pamoja na ukaguzi wa mara kwa mara wa watoa huduma za ndege chini ya mfumo wa udhibiti wa TCAA na kwa mujibu wa Kanuni za Usafiri wa Anga kuhusu Uthibitishaji na Usimamizi wa Watoa huduma za Ndege za mwaka 2017.
(b) Kwa taarifa zaidi kuhusu utaratibu wa maombi na uthibitishaji wa Cheti cha Utoaji huduma za Ndege (AOC), bofya hapa
2. UTOAJI WA LESENI (LICENSING)
(a)Ofisi ya Uendeshaji wa Ndege hushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Leseni za Wataalamu wa Anga katika utoaji rasmi na usimamizi wa leseni na vyeti vya wataalamu wa anga. Hii inajumuisha:-
- Marubani;
- Wahudumu wa ndani ya ndege (Cabin Crew);
- Maofisa wa kupanga safari za ndege (Flight Dispatchers);
- Waendeshaji wa droni (Drone Operators).
(b)Ofisi ya Uendeshaji wa Ndege kwa kushirikiana na Ofisi ya Leseni za Wataalamu wa Usafiri wa Anga hutathmini maombi ya leseni za kigeni kwa ajili ya kubadilishwa au kuthibitishwa kuwa leseni za Tanzania kwa kushauriana na nchi nyingine wanachama wa ICAO.
(c)Kitengo hiki pia hutoa na kuhuisha leseni, vyeti pamoja na daraja za ziada za ujuzi kwa wataalamu wa sekta ya anga.
3. MAFUNZO
Shirika lililoidhinishwa la Mafunzo (Approved Training Organization – ATO)
Ofisi ya Uendeshaji wa Ndege hushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Leseni za Wataalamu wa Usafiri wa Anga katika kufanya uthibitishaji, utoaji wa vibali na usimamizi wa Mashirika Yaliyoidhinishwa ya Mafunzo (Approved Training Organizations – ATOs) kwa mujibu wa Kanuni za Usafiri wa Anga kuhusu Mashirika Yaliyoidhinishwa ya Mafunzo za mwaka 2017 [Civil Aviation (Approved Training Organizations) Regulations, 2017] kupitia:-
(a)Kuidhinisha mashirika ya mafunzo;
(b)Kuthibitisha vifaa vya mafunzo ya uigaji wa uendeshaji ndege (flight simulation training devices);
(c)Kufanya ufuatiliaji endelevu wa mashirika yaliyoidhinishwa ya mafunzo.
4. MASUALA YA KIUDHIBITI
(a)Ofisi ya Uendeshaji wa Ndege huandaa na kusimamia kanuni zinazohusiana na uendeshaji wa ndege, ikiwamo uandishi wa kanuni, marekebisho ya kanuni pamoja na nyaraka za mwongozo wa kiufundi (Technical Guidance Materials – TGMs).
(b)Kusimamia utekelezaji wa sheria na kanuni.
(c)Kuandaa taratibu za utekelezaji.