TANZANIA NA MOROCCO ZAIMARISHA USHIRIKIANO WA USAF...

TANZANIA NA MOROCCO ZAIMARISHA USHIRIKIANO WA USAFIRI WA ANGA

18 Novemba, 2026
TANZANIA NA MOROCCO ZAIMARISHA USHIRIKIANO WA USAFIRI WA ANGA

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ufalme wa Morocco zilifanya kikao cha cha mawaziri wa nchi hizo mbili tarehe 17 Novemba 2026 jijini Montréal, Canada, wakati wa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Usafiri wa Anga (ATConf/7), unaoendelea kuanzia tarehe 16 hadi 20 Novemba 2026. Kikao hicho kililenga kuimarisha ushirikiano katika usafiri wa anga, kuboresha miunganiko ya safari za ndege na kuendeleza utekelezaji wa Makubaliano ya Huduma za Usafiri wa Anga kati ya nchi hizo mbili (BASA), yaliyosainiwa mwaka 2016.

Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Mheshimiwa Dkt. Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Miundombinu na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ujumbe wa Morocco uliongozwa na Mheshimiwa Abdessamad Kayouh, Waziri wa Uchukuzi na Lojistiki wa Ufalme wa Morocco.

Dkt. Mohamed alieleza kuwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limeonesha nia ya kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Casablanca mwaka 2027. Alibainisha kuwa njia hiyo inaweza kuimarisha miunganiko ya safari za ndege kati ya Afrika Mashariki na Afrika Kaskazini, kukuza utalii, kurahisisha biashara na kupanua fursa za kufikia masoko ya kimataifa.

Aidha, Dkt. Mohamed alipendekeza kuundwa kwa kikosi kazi cha pamoja cha kiufundi kitakachojumuisha mamlaka za usafiri wa anga na wadau husika kutoka nchi zote mbili. Kikosi hicho kitaratibu mashauriano, kitashughulikia mahitaji ya kiutendaji na ya kikanuni, na kitaandaa mpango wa hatua za kuanzisha huduma za moja kwa moja.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Kayouh alieleza kuwa Morocco hupokea takribani watalii milioni 19 hadi 20 kwa mwaka. Alisema kuwa kuongezeka kwa mahitaji ya safari za kimataifa kunatoa fursa ya kuboresha miunganiko ya safari za ndege kati ya Morocco na Tanzania na kukuza utalii, biashara na uwekezaji.

Kikao hicho kiliendeleza mazungumzo kuhusu pendekezo la kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Casablanca. Majadiliano hayo yaliendana na malengo ya ATConf/7 ya kuimarisha miunganiko ya safari za ndege za kimataifa na kukuza sekta ya usafiri wa anga kwa njia endelevu.

Unahitaji Msaada?