Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeibuka mshindi wa kwanza na kutunukiwa tuzo ya utendaji bora miongoni mwa taasisi za usimamizi (Regulatory Authorities) zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi.
Tuzo hiyo imekabidhiwa Novemba 17, 2026, na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb.), na kupokelewa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TCAA, Bi. Mtumwa Ameir.
Hafla hiyo imefanyika wakati wa Mkutano wa 19 wa Tathmini ya Utendaji wa Sekta ya Uchukuzi (Joint Transport Sector Review Meeting – JTSR) kwa mwaka wa fedha 2025/26, unaofanyika kuanzia tarehe 16 hadi 18 Novemba 2026, katika Ukumbi wa Malaika Beach Resort, jijini Mwanza.
Mkutano huo unawakutanisha viongozi wa Serikali, taasisi zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi na wadau mbalimbali kwa lengo la kutathmini mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa mipango na miradi ya sekta ya uchukuzi, pamoja na kuweka mikakati ya kuimarisha utendaji na maendeleo ya sekta hiyo nchini.