Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeshiriki Mashindano ya 56 ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA 2026), yaliyofanyika mkoani Morogoro. Mamlaka imeshiriki katika michezo mbalimbali ikiwemo mchezo wa jadi wa bao, karata, drafti, mbio fupi na mashindano ya baiskeli, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuendeleza ustawi wa watumishi, kuimarisha mshikamano na kukuza tija kazini.
Akifungua rasmi mashindano hayo tarehe 12 Novemba 2026, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewahimiza watumishi wa taasisi za umma na sekta binafsi kushiriki michezo na kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara ili kuimarisha afya, kujikinga na magonjwa na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao. Aidha, amezipongeza taasisi na makampuni yaliyoshiriki, akibainisha kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kujenga umoja, kuimarisha mshikamano na kukuza mahusiano mazuri miongoni mwa watumishi.
Katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Dkt. Jabiri K. Bakari, aliwakilishwa na Mkurugenzi wa Huduma za Mamlaka (DCS), Bw. Lembris Laanyuni, ambaye alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na watumishi wa TCAA wanaoshiriki mashindano hayo katika michezo mbalimbali. Mkutano huo ulionesha uungwaji mkono wa uongozi wa Mamlaka kwa ushiriki wa watumishi katika michezo na kusisitiza utambuzi wa TCAA kuhusu umuhimu wa afya ya mwili na akili katika kujenga nguvu kazi yenye afya, ari na tija.