Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeshiriki katika Mkutano wa 19 wa Tathmini ya Utendaji wa Sekta ya Uchukuzi (Joint Transport Sector Review Meeting – JTSR), uliofanyika kuanzia Novemba 16 hadi 18, 2026, katika Ukumbi wa Malaika Beach Resort, jijini Mwanza.
Mkutano huo, ulioandaliwa na Wizara ya Uchukuzi, umefunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba. Hafla hiyo pia imehudhuriwa na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Mwakiposa Kihenzile, pamoja na viongozi wengine wa Serikali na wadau mbalimbali wa sekta ya uchukuzi.
Ujumbe wa TCAA katika mkutano huo umeongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Bi. Mtumwa Ameir, huku Mkurugenzi Mkuu wa TCAA akiwakilishwa na Mkurugenzi wa Huduma za Uongozaji Ndege, Mha. Flora Alphonce. Katika mkutano huo, Mha. Alphonce aliwasilisha mada kuhusu utendaji wa sekta ya usafiri wa anga nchini kwa mwaka wa fedha 2025/2026, akieleza maendeleo yaliyopatikana, mafanikio yaliyofikiwa, changamoto zilizojitokeza pamoja na mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa Taifa.
Mkutano huo ni jukwaa muhimu la kutathmini utekelezaji wa mipango na miradi ya sekta ya uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kubaini mafanikio na changamoto zilizopo, pamoja na kujadili mikakati ya kuboresha ufanisi na kuimarisha utoaji wa huduma katika sekta hiyo. Aidha, tathmini hiyo inalenga kuhakikisha mipango na vipaumbele vya sekta vinaendana na mwelekeo wa maendeleo ya Taifa, hususan Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.